CUF Yataka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Awaombe Radhi Watanzania Kwa Kuwadhalilisha

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja


Chama cha Wananchi(CUF) kimemtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awaombe radhi watanzania kwa kuwadhalilisha kuwa hawapendi kufanya kazi, badala yake  wanashinda kuangalia Bunge, hali ambayo imeisababisha lisirushwe moja kwa moja.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF Taifa, Twaha Taslima amesema Waziri Mkuu alitoa tuhuma hizo kwa wananchi akiwa nchini Marekani hivi karibuni,wakati  siyo kweli kwamba watanzania wanakesha kuangalia bunge tangu  linapoanza hadi linakwisha bila kufanya kazi.

Hivi karibuni Waziri Majaliwa akizungumza na watanzania waishio Uingereza alisema sababu ya bunge kutorushwa moja kwa moja ni kutekeleza kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’

“Kama ni hivyo basi maisha ya watanzania wengine yangekwama hivyo Serikali ya awamu ya tano kazi yake kubwa sasa ni kutaka kuwarudisha watanzania kwenye woga wa kutoiwajibisha Serikali kwa kisingizio cha hapa kazi tu slogani hii ni ya kuua demokrasia,” amesema Taslima.

Taslima ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu hali ya demokrasia nchini na mwelekeo wa CUF baada ya Uchaguzi.

Amesema kuna madhara mengi katika kukandamiza demokrasia, ikiwamo wananchi kujenga chuki na Serikali, hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo.

Taslima ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi waliowezesha chama hicho kuongeza idadi ya wabunge kutoka 34 mwaka 2010 hadi 42 katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.

Amesema CUF baada ya kumaliza shughuli za uchaguzi inajipanga kufanya ziara nchi nzima, lakini pia inajiandaa na uchaguzi wa kuziba mapengo ya uongozi ngazi mbalimbali kuanzia kwenye matawi hadi taifa.

“ Kwa sababu tofauti baadhi ya nafasi za uongozi badi zipo wazi  hivyo  ndani ya kuipindi cha miezi miwili ijayo tunatarajia kujaza nafasi hizo, wakati ile ya Mwenyekiti wa taifa ambaye alijiuzulu itajazwa Agosti chama kitakapoitisha mkutano mkuu wa taifa,” amesema.

Akizungumzia kuhusu ushirikiano ulivyo baina ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Taslima alisema umoja huo ulishinikizwa na wananchi walioichoka CCM, hivyo walihitaji vyama hivyo viunganishe nguvu ili kushika dola.

“Lakini ni wazi kwamba sheria hairuhusu kuungana hivyo UKAWA tupo nje ya sheria lakini hatujavunja sheria, sasa tunafikiria kuanza kufanya mchakato wa kujijenga ndani ya misingi ya sheria kwa chaguzi zijazo,”
amesema Taslima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Sheweji Mketo amesema ushindi wa majimbo 10 walioupata unatokana na tathimini ambayo waliifanya mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.

“Baada ya uchaguzi ule kupita tulifanya CUF tulifanya tathimini ambapo tulibaini kwamba kuna majimbo 54 ambayo CCM licha ya wananchi kuichoka, lakini ilishinda kwa sababu kulikuwa na wagombea wengi wa vyama vya upinzani hali iliyosababisha kushindwa suluhisho lilikuwa ni kuungana,” amesema .

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI