Mizengo Pinda ( Mtoto wa Mkulima ) Aishi Maisha ya Kikulima

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, maarufu kama Mtoto wa Mkulima, ameamua kuishi maisha tofauti kabisa na watangulizi wake kwa kukwepa kukaa jijini Dar es Salaam na kwenda kijijini kwake baada ya kustaafu.Pinda aliwahi kukiri kwamba hana nyumba jijini Dar es Salaam zaidi ya kibanda kidogo kilichoko Pugu, ambacho hakina hadhi ya kuishi mtu.

Mtoto huyo wa mkulima amejichimbia katika kijiji cha Makanyagio, Mpanda mkoani Katavi, akiendesha shughuli za kilimo na ufugaji, tofauti kabisa na watangulizi wake ambao baada ya kustaafu waliendelea kuishi jijini Dar es Salaam.

Tangu awamu ya nne ilipoondoka Ikulu Novemba 5, mwaka jana, Pinda hajawahi kufanya safari yoyote nje  ya nchi na wala kujihusisha na shughuli za kitaifa na kijamii kama walivyokuwa watangulizi wake.

Aidha, Mizengo Pinda amepotea kwenye vyombo vya habari kama watangulizi wake.

Mtoto wa Mkulima ni jina ambalo alijipachika mwenyewe baada ya kuteuliwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2008 kuwa Waziri Mkuu.

Pinda alikuwa Waziri Mkuu kati ya mwaka 2008-2015 akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Edward Lowassa (2006-2008), aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

Wakati Salim Ahmed Salim, baada ya kustaafu, aliendelea kuishi kwenye makazi yake Masaki na Unguja, John Malecela naye aliendelea kuishi Sea View, Upanga.

Fredrick Sumaye baada ya kustaafu nafasi hiyo mwaka 2005 aliendelea kuishi jijini Dar es Salaam maeneo ya Kiluvya, wakati Lowassa bado ana makazi Masaki.

Jaji Joseph Warioba, ambaye naye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliendelea kuishi nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam baada ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo mwaka 1990.

Hata Waziri Mkuu mstaafu, hayati Rashid Kawawa aliweka makazi yake ya kudumu eneo la Madale jijini Dar es Salaam na ndiko alikozikwa alipofariki Desemba 2009.

Cleopa Msuya anaendelea kuishi kwenye makazi yake yaliyoko Upanga, jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Pinda alikuwa miongoni mwa wanachama 42 wa CCM waliochukua fomu za kuwania kuteuliwa na chama chao kusimamishwa kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Lakini bahati haikuwa kwake kwani ni miongoni mwa makada ambao majina yao yalikatwa mapema na Kamati Kuu ya chama hicho, hivyo kutofanikiwa hata kuingia kwenye tano bora.

Wanachama wa chama hicho walioingia kwenye tano bora walikuwa Rais John Magufuli, January Makamba, Benard Membe, Dk. AshaRose Migiro na Amina Salum Ali.

Tangu kukatwa jina lake kwenye hatua za awali, Pinda alionekana kujitenga kabisa na masuala ya siasa na kuamua kuishi maisha tofauti na wenzake baada ya kustaafu.

Januari 14, 2010 Pinda alitangaza mali anazomiliki kuwa ni Sh. milioni 25 kwenye akaunti yake, nyumba tatu za kawaida moja ikiwa jijini Dar es Salaam, Mpanda na Dodoma na gari moja alilolinunua kwa mkopo wa Ubunge.

Waziri Pinda aliamua kufanya hivyo ili kuweka bayana mali zake na kuonyesha mfano kwa viongozi wote nchini kufata nyayo kwa kuwa viongozi walitakiwa kuweka bayana mali zao ili kutekeleza sheria ya maadili ya uongozi.

Pinda alisema haelewi maana ya utajiri na kwamba mali alizotaja zimeshamtosheleza.

"Nina nyumba Dodoma ninayojenga kwa mikopo ya nyumba za serikali," alisema Pinda mwaka huo na kueleza zaidi:

"Nina nyumba Mpanda ambayo imepatikana kwa mpango wa kawaida tu, imetokana na visenti kidogo nikanunua pale ambapo bahati nzuri gharama za ujenzi hazikuwa kubwa sana, nikakikarabati kipo pale kipo Makanyagio pale.

"Haya! Ukitoka pale unataka niseme nini tena. Dar es Salaam sina nyumba ya kusema ya maana sana ukienda shambani Pugu kule kipo kinyumba kidogo hivyo inahitajika kazi ya ziada kuweza kufanya paonekane pa maana.

"Kijijini kwa baba yangu pale Kibaoni sina nyumba; pale mlipoona nimekaa na bibi tunapiga porojo, kile kijumba mimi na wadogo zangu tulimsaidia babu kwa ajili ya kumjengea babu yetu na pale ndipo nilipokuwa nafikia siku zote wakati wa likizo."

Pinda, ambaye alikuwa Mbunge tangu mwaka 2000 mpaka 2015, alisema miaka yote alikuwa akifikia kwenye nyumba hiyo ambayo yeye ana chumba chake kimoja hali kadhalika babu yake.

Alisema baada ya kuwa Waziri Mkuu, alijikuta kwenye wakati mgumu sana kwa kuwa alitaka kuendelea kufikia kwenye nyumba hiyo, lakini watu wa usalama walimkataza.

"Nilipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu nikataka nifikie katika ile nyumba, lakini nikaambiwa hapana, haiwezekani; hapafai; huwezi kufikia pale," alisema.

Alisema hilo ndilo lilikuwa tatizo lake la kwanza kwa hiyo atajaribu kujenga tena kitu ambacho na yeye atapata mahala pa kufikia pamoja na wasaidizi wake kwenye eneo hilo wakati huo.

"Nimegundua tatizo ni hawa wakubwa. Pale kijijini kwetu hakuna nyumba za wageni hatuna chochote mi nilidhani nikienda kule nikiachwa kwa babu na bibi, wao wataenda huko umbali wa kilomita wakatafute pa kupumzika, lakini wakasema no! no! no! haiwezekani, nikawaelewa."

Alisema ukiondoa nyumba hiyo, vitu vya maana zaidi hana labda gari la mkopo akiwa Mbunge.

"Hivi ukiwa na hivi nilivyo navyo unahitaji nini cha zaidi tena?

"Kwa hiyo kipato kidogo unachokipata unaweza kukitumia kwa ajili ya huduma za watoto wako kusoma na kadhalika kwa sababu ni vitu viko nje ya taratibu za serikali.”

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI