Samia: Sijawahi Kupinga Utumbuaji Majipu, Lakini Nilishauri Wakuu wa Mikoa Wazingatie Sheria Kabla ya Kumfukuza Mtu

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma wanapotaka kuwafukuza watumishi wasio waadilifu.

Alisema hajapinga kauli ya Rais John Magufuli ya kutumbua majipu kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, hivi karibuni kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani.

Samia aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, wakati akisisitiza zoezi la kuhamisha mifugo iliyopo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Alisema wakuu wa mikoa na wilaya nchini, wanapaswa kuhakikisha wanapotaka kuwawajibisha watumishi wa umma wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Aliongeza kuwa mwenye mamlaka ya kutumbua majipu ni Rais pekee, kwa sababu anateua, anaajiri na kufukuza kwa hiyo viongozi wengine wakiwamo wakuu wa mikoa na wa wilaya wafuate taratibu.

“Rais pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuteua, kutengua na kuajiri lakini sijapinga utumbuaji majipu, bali nasisitiza kila mkuu wa mkoa na DC (mkuu wa wilaya) afuate sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma,” alisema Samia.

Makamu wa Rais, aliwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha mifugo ya nje ya nchi iliyopo hifadhini inaondolewa ifikapo Juni 30.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela alishukuru Tanapa kwa kuwapa msaada madawati ili kupunguza kero ya wanafunzi kukaa chini.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera alisisitiza kuwa atahakikisha mkoa wake unapunguza migogoro ya ardhi ili hifadhi za Taifa ziweze kulindwa, huku wananchi wakiheshimu na kulinda mipaka ya hifadhi na rasilimali za Taifa.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI