Tanzania Kuwa Nchi Ya kwanza Duniani Kutumia Kitambaa Kilichowekewa Viatilifu Kudhibiti Malaria

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja


Tanzania imekuwa nchi ya kwanza duniani kufanya majaribio ya kupambana na mbu waenezao magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria kwa kutumia kitambaa kilichowekewa viatilifu ili kudhibiti ugonjwa malaria ambao ni tishio kwa afya ya wananchi wengi wanaoishi vijijini.


Hatua hiyo ya utafiti imefikiwa na watafiti wa magonjwa ya binadamu katika cha taifa cha Magojwa ya Binadamu (NIMR) katika kituo cha Amani mkoani Tanga ili kuweza kuwadhibiti mbu waenezao ugonjwa malaria ambao unaathiri watu wa rika zote nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani Tanga Dkt. William Kisinza alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kutoka Kituo cha Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani ambao walitembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki kujionea namna Tanzania inavyopambana na ugonjwa huo.

Katika kufanikisha majaribio hayo, Dkt. Kisinza amesema kituo hicho kinaendelea vizuri na majaribio ambapo wanatarajia mchanganuo wa utafiti huo utafanyika mwishoni mwa mwaka 2016 na taarifa kamili itatolewa rasmi mwaka 2017 ili iweze kutumika nchi nzima na duniani kote.

Dkt. Kisinza amesema kuwa mafanikio ya taasisi yake yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo na taasisi nyingine za kitaaluma ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Afya cha Kilimanjaro (KCMC), Kituo cha Kudhibiti Kuzuia na Magonjwa cha Marekani (CDC), Taasisi ya Tiba, Dawa na usafi wa mazingira ya London nchini Uingereza (LSHTM) na Chuo Kikuu cha Brandeis cha nchini Marekani.

Naye Mtafiti Mkuu anayesimamia zoezi la majaribio hayo ya mradi huo wa vitambaa vyenye viatilifu hivyo vijulikanavyo kama “insecticide treated wall liners”, Dkt. Joseph Mugasa amesema kuwa zoezi hilo linahusisha vijiji 44, kaya zaidi ya 25,000 na idadi ya watu wanaonufaika na majaribio hayo ni zaidi ya 100,000 katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Mbali na kuangalia uwezo wa vitambaa hivyo, mradi huo unaangalia pia uwezo wa vitambaa hivyo katika kukabiliana na upugufu wa damu kwa watoto chini ya miaka 11, uwezo wa vitambaa kupambana na mbu sugu kwenye viatilifu vingine na pia kufanya tathmini ya gharama anazoingia mwananchi katika kugharamikia tiba za malaria.

Kitambaa hicho ambacho huwekwa kwenye kuta za nyumba kwandani hutumika sambamba na chandarua ili kuweza kutoa kinga madhubuti mara mbili kumkinga binadamu dhidi ya mbu waenezao magonjwa.

Mradi huo wa majaribio wa kutokomeza ugonjwa wa malaria umeanza kufanyiwa utafiti nchini miaka mtatu iliyopita kuanzia 2013 na unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) chini ya Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Malaria (PMI) ambao hadi kukamilika kwake utarajiwa kugharibu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 3.

Kwa upande wake Meneja wa Mawasiliano Taasisi ya “Malaria No More” ya nchini Marekani ambaye pia ni Mkuu wa msafara wa waandishi hao Dena Gudaitis amesema kuwa wamefurahishwa kuona Tanzania ilivyosimama imara kujali afya za wananchi wake hasa watu wa kipato cha chini ambao wengi wao wanaishi vijijini.

Katika kutekeleza wajibu wao wa kiuandishi, waandishi hao kutoka ICFJ wanaongozwa na kaulimbiu ya taasisi hiyo inayosema “Andaa mazingira bora ya mwandishi wa habari wa kimataifa ajaye”.

Waandishi hao wa habari wamefanya ziara ya siku tano nchini kuanzia Mei 8 hadi 13, 2016 katika mikoa ya Dar es salaam, Arusha na Tanga ambapo wametembelea baadhi ya zahanati katika mikoa hiyo, familia zenye watoto walio chini ya mpango wa majaribio wa kudhibiti malaria, vituo vya utafiti vya Korogwe na Amani pamoja na kiwanda cha kutengenezea vyandarua cha A to Z cha jijini Arusha.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI