Waliotapeli Bilioni 62 Uingereza Waanza Kusakwa Jijini Dar es Salaam

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja

Shirika la Kimataifa la Polisi linawasaka raia wawili wa Scotland wanaodaiwa kukimbilia Tanzania baada ya kufanya udanganyifu na kujipatia Paundi 20 milioni za Uingereza (sawa na Sh62 bilioni). 

Wawili hao, Gareth Johnson (48) na Geoffrey Johnson (72) walikuwa sehemu ya kundi la watu 18, lililohusishwa na uhalifu huo wa uchakachuaji ongezeko la kodi ya simu za mkononi nchini Uingereza.

Kutokana na kosa hilo, Mahakama Maalumu ya Mapato na Forodha ya Uingereza (HMRC) iliamuru wanafamilia hao, ambao ni baba na mwanae, walipe fidia ya Paundi 109 milioni (sawa na Sh337 bilioni).

Lakini hukumu hiyo ilitoka bila ya wawili hao kuwapo baada ya kutoroka kabla ya shauri hilo kuanza kusikilizwa na inasemekana walikimbilia Tanzania.
Akizumgumzia suala hilo, Mkuu wa Interpol Tanzania, Gustavus Babile alisema kibali cha kimataifa cha kukamatwa kwa wawili hao kipo kwenye tovuti yao.

Alisema walipokea taarifa kutoka Uingereza hivyo hatua inayofuata ni kukipeleka kibali hicho mahakamani kwa ajili kupata nguvu za kisheria za nchi.

Balile alisema baada ya hatua hiyo, utafanyika uchunguzi ili kubaini kama watuhumiwa hao wapo nchini. “Kama wapo watakamatwa,” alisema.

Picha na majina ya raia hao wa Scotland zimebandikwa kwenye tovuti ya Interpol kwa kuwekewa bendera nyekundu, ikiwa ni alama ya kusakwa na polisi hao wa kimataifa.

Awali, alipoulizwa kuhusu hilo, msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema litashughulikiwa baada ya Uingereza kutoa taarifa ya watuhumiwa hao.

Hadi sasa inadaiwa kuwa Geoffrey na kijana wake wamekuwa “mafichoni” Tanzania kwa takriban miaka mitatu sasa. 
Mapema Aprili mwaka huu, Gazeti The Mirror la Uingereza liliripoti kuwa wawili hao, ambao wametakiwa kulipa fedha hizo mara moja au waongezewe adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela, wamebainika kuwapo nchini.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa makazi yao mara baada ya kufika nchini yalikuwa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakati uchuguzi huo ukibaini hilo, mienendo yao inaonyesha kuwa kwa sasa wapo mkoani Iringa.

Inadaiwa kuwa Geoffrey, ambaye Mahakama iliamuru afungwe jela miaka 10 katika hukumu ya mwaka 2014, ni wamiliki wa kampuni ya Johnson International Group ambayo makazi yake ni Kipawa jijini Dar.

Kampuni ya Johnson, ambayo inasimamiwa na kijana wake ambaye pia alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela, imeajiri wafanyakazi 125.

Lakini, taarifa ya gazeti hilo kwenye mtandao wake, inaeleza kuwa kampuni hiyo haina uhusiano mzuri na wafanyakazi wake kwa sababu haijawalipa mshahara kwa muda mrefu. 
Kutokana na mvutano uliokuwapo kati wa wafanyakazi hao na waajiri wao, wafanyakazi 40 walipeleka madai yao kwa mkuu wa mkoa mwaka 2014.

Pia, wafanyakazi hao walidai kunyanyaswa hasa pale walipoomba kuongezwa mshahara huku mwajiri wao akiwatishia kuondoa michango yao ya pensheni.

Mmoja wa wasimamizi wa kampuni ya Johnson, Leonard Lukule alisema hali hiyo imesababishwa na hali mbaya ya kiuchumi ndani ya kampuni.

“…Kuna wakati tulilazimika kutoa likizo za lazima kwa wafanyakazi,” alisema Lukule.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI