Wanaharakati na Wanasiasa Waaswa kuacha kubeza Mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano Chini ya Rais Magufuli

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja


Wanaharakati na wanasiasa wanaobeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano, wametakiwa kuacha kuupotosha umma juu ya mafanikio yaliyofikiwa na Serikali hiyo chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam leo na Afisa Habari wa CZI- information And Media Consults Co. Ltd, Augustino Matefu  wakati wa mkutano na vyombo vya Habari uliolenga kueleza mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imeonesha mafanikio makubwa katika sekta ya ukusanyaji mapato, elimu, miundombinu, afya na kujenga uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma.

Hivyo alitoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano na kuwapuuza wanaharakati na wanasiasa hao wanaunga mkono wale wasioitakia mema Tanzania na Serikali ya awamu ya tano kwa ujumla.

Alisema katika sekta ya mapato, Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miezi saba iliyopita imefanikiwa kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 900 kwa mwezi kabla ya utawala wake hadi shilingi trilioni 1.5 kwa sasa.

 “Rais wa awamu ya tano ameondoa michango yote ya shule za msingi na Sekondari ambayo ilikuwa kero kwa wazazi na wananchi kwa ujumla” alisisitiza Matefu

Katika mpango wa elimu bure Matefu alibainisha kuwa umesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kujiunga na elimu ya msingi na ile ya Sekondari.

Aliongeza kuwa Rais Magufuli amejenga Barabara ya Mwenge hadi Moroko kwa Fedha za ndani hali inayoonyesha kuwa Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo  wananchi wake.

Alisema hata Hosipitali ya Taifa Muhimbili imepatiwa  vitanda vya kutosha na hivyo kuondoa tatizo la msongamano katika wodi ya wazazi na kwa sasa wagonjwa wanalala kwenye vitanda.

“Mambo mengine yaliyofanywa na Serikali katika kipindi hiki yanalenga kuinua maisha ya wananchi wa chini ikiwemo kujenga mazingira mazuri yatakayowezesha shughuli za uzalishaji kuongezeka ili kuinua hali ya maisha ya wananchi” alisema Matefu.

Kujengwa kwa utamaduni wa uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma ni moja ya mambo yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano ambapo sekta ya utumishi wa umma imeonesha mabadiliko makubwa katika uwajibikaji.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI