Rais Magufuli kuhutubia mkutano wa hadhara Jumapili Wilayani Kahama

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja


Rais John Magufuli anatarajia kufanya ziara wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako atafanya mkutano wa hadhara kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliopita. 
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulu alisema jana kwamba Rais Magufuli atawasili hapa Jumamosi jioni kabla ya kufanya mkutano wa hadhara Jumapili. 
Nkulu aliwataka wananchi wa Kahama na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo katika ziara hiyo ambayo alisema: “Lengo lake ni kuwapongeza wananchi wa Kahama kwa kumpa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika mwaka jana.” 
Alisema ziara hiyo ni muhimu kwa kuwa ni ya kwanza mkoani Shinyanga akianzia na Kahama. 
“Tujipongeze wananchi kutokana na kupata bahati ya wilaya chache zilizotembelewa na kiongozi huyu, Kahama imekuwa mojawapo,” alisema Nkulu. 
Alisema kwa kuwa Jumamosi ni siku ya usafi kitaifa, kila mmoja wilayani humo ahakikishe anaweka mazingira katika hali ya usafi na kuwaonya wafanyabiashara kuwa atakayeshindwa kufanya hivyo hataruhusiwa kufungua biashara. 
“Nitafanya ukaguzi Jumamosi kuhakikisha kila mtu anashiriki usafi. Hilo ni agizo la kitaifa kwa sasa lazima kila mmoja awajibike, nimewaagiza watendaji wote wa kata kusimamia hilo,” alisema Nkulu. 
Alisema wananchi watatangaziwa ratiba yote ya Rais Magufuli kwenye gari la matangazo ambalo litazunguka mji mzima wa Kahama kuwaeleza muda na eneo ambalo kiongozi huyo atafanyia mkutano.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI