Tanzania Yachaguliwa Kuongoza Mkutano Wa Kimataifa Wa Wamiliki Wa Kampuni

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja

Kufuatia uchumi wa Tanzania kuzidi kukua na kushika nafasi ya kwanza kwa ukuaji uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na jitihada zake za kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda.

Imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa Chama cha Kampuni Ndogo na za Kati Ulimwenguni unaotarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 5 hadi 7, 2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julias Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye amesema chama hicho huchagua nchi yenye uchumi mkubwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kwamba kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wake, kunaashiria kuwa miongoni mwa nchi inayokuwa kiuchumi kwa kasi barani Afrika.

“Tanzania sasa inaanza kuonekana kuwa na hadhi, hali hii huenda inachangiwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli, na itakuwa nchi ya tatu kufanyika mkutano huo unaokutanisha wadau na wamiliki wa kampuni ndogo na za kati duniani,” amesema.

Amesema mkutano huo utasaidia kampuni za ndani kujifunza namna ya kutoka katika kampuni ndogo kwenda za kati na za kati kuwa kubwa.

Amesema pia TPSF itaitumia fursa hiyo kutangaza kwa wageni fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

“Mkutano huo pia utafungua milango ya biashara sababu tunatarajia wageni zaidi ya 200 kutoka nje, watahitaji malazi, chakula na hata bidhaa nyingine za ndani. Pia tutawaomba wahudhurie katika maonyesho ya bidhaa za Tanzania yatakayoanza Disemba 7 hadi 11, 2016 ili wajionee bidhaa zinazozalishwa nchini,” amesema.

Simbeye amesema kuwa, tafiti iliyofanywa na serikali mwaka 2013 na kuchapishwa mwaka huu inaonyesha kuwa kuna viwanda 49,000 ambapo 20,000 ni viwanda vikubwa.

“Uchumi wa Tanzania utajengwa na viwanda hasa vidogo ambavyo vitaongeza idadi ya kampuni ndogo nchini, nchi inapokuwa na kampuni nyingi fursa za kiuchumi pia huongezeka sababu zinaajiri watu. Taasisi ya Sekta Binafsi itaendelea kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizomo nchini,” amesema.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI