CUF Yakubali Kushiriki Uchaguzi wa Mbunge Dimani, Mwaka jana Walisusa Baada ya Jecha Kufuta Matokeo

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja


Kamati ya Utendaji ya CUF imepitisha majina matatu ya wanaowania kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Dimani, Mkoa wa Mjini Mgharibi kisiwani Unguja. 
 
Wakati CUF imepitisha majina hayo yatakayokwenda kwenye mchujo wa kura ya maoni ndani ya chama hicho kupata jina moja, CCM nao wamepitisha majina matatu ambayo ni Juma Ali Juma, Hussein Migoda Mataka na Abdalla Sheria yatakayopitia mkondo huohuo. 
 
Uchaguzi huo utakaofanyika Januari 22, mwakani umetangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), kujaza nafasi ya Hafidh Ali Tahir aliyefariki dunia ghafla mkoani Dodoma hivi karibuni wakati akihudhuria vikao vya Bunge. 
 
 CUF itakuwa ikishiriki uchaguzi huo kwa mara ya kwanza baada ya kususa ule wa marudio uliofanyika Machi 20, kutokana na kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana. 
 
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alitaja majina hayo kuwa ni Abdulrazak Khatib Ramadhan, Asha Hamad Makungu na Ahmed Abass Haji, ambao watapigiwa kura jimboni huko ili kumpata mmoja atakayeiwakilisha CUF. 
 
Akizungumza baada ya kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, Mazrui alisisitiza kuwa chama hicho hakitazikubali hujuma zote, yakiwamo masharti hayo ya NEC aliyoyaita ya mfukoni. 
 
Katika hatua nyingine, CUF imesema inaendelea na mazungumzo na vyama vinavyounda Ukawa kuona namna bora ya kushiriki uchaguzi mdogo ujao jimboni humo ili kuhakikisha wanaibwaga CCM. 
 
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Joram Bashange alisema chama hicho bado ni sehemu ya Ukawa na hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kutengua uamuzi huo. 
 
“Suala hilo lilipitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa uliofanyika tarehe 23 mpaka 27 Juni, 2014 na mkutano mkuu ndicho chombo cha juu kabisa na chenye maamuzi ya mwisho katika chama,” alisema. 
 
Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa madiwani 22 Tanzania Bara na ubunge wa Dimani. 
 
Kamati ya Utendaji ilipitisha ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama kwa ajili ya kuwapata wagombea wa CUF katika nafasi hizo. 
 
Wakati huo huo, Bashange amesema Kamati ya Utendaji ya Taifa imeshangazwa na kauli ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima kwamba wagombea wa CUF lazima fomu zao za uteuzi zithibitishwe na kutiwa saini na pande mbili zinazohasimiana. 
 
“Kailima amekitoa wapi kifungu cha sheria au kanuni, alichokitumia kuweka sharti hilo la ajabu tena kwa chama kimoja tu,” alisema na kuongeza:“Huwezi kuwa na sharti linalokihusu chama kimoja tu katika kuthibitisha uteuzi wa wagombea.” 
 
Alisema fomu za uteuzi wa wagombea kutoka NEC huthibitishwa na katibu wa chama wa ngazi inayohusika na kwa ubunge na madiwani ni katibu wa wilaya.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI