Washitakiwa Wanne Mauaji wa Dr. Mvungi Waachiwa Huru

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru washitakiwa wanne kati ya 10 waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya bila  kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi.

Washitakiwa walioachiwa ni Masunga Makenza (40), mkazi wa Tabata Darajani, Zacharia Msese (33), Ahmad Kitabu (30) mkazi wa Mwananyamala na John Mayunga (56).

Waliachiwa kwa mujibu wa Kifungu Namba 91 Kifungu kidogo cha kwanza cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Wakili wa Serikali, Pamela Shinyambala alidai mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba kuwa upande wa mashitaka umeshasajili jalada hilo Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mshitaka Nchini (DPP), hakuwa na nia ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao kwa mujibu wa kifungu hicho. Awali, Shinyambala alidai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutolewa maelezo ya mashahidi baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Hakimu Simba alisema anawaachia washitakiwa hao, kama walivyoomba upande wa mashitaka. Alisema kwamba washitakiwa sita, ndio watakaosomewa maelezo hayo ya mashahidi.

Washitakiwa hao ni Longishu Losingo (29), Paulo Mdonondo (30) mkazi wa Tabata Darajani, Mianda Mlewa (40) Mkazi wa Vingunguti, Juma Kangungu (29) mkazi wa Vingunguti, Msungwa Matonya (30), mkazi wa Vingunguti na Masenga Mateu.

Hata hivyo, Hakimu Simba aliutaka upande wa mashitaka, kuhakikisha kwamba wanaleta cheti cha kifo cha mshitakiwa wa kwanza, Chibago Magozi (32), mfanyabiashara mkazi wa Vingunguti Machinjioni.

Pia alieleza kuwa kesi hiyo ikienda mahakama kuu, bila ya kupelekwa mahakamani hapo cheti cha kifo, itakwama kwa kuwa hawawezi kusoma maelezo hayo hadi kwa mtu aliyekufa.

Aliwataka kuhakikisha katika tarehe ijayo ambapo washitakiwa sita watasomewa maelezo, wawe wamewasilisha cheti cha kifo.

Hata hivyo, Wakili Shinyambala alikubaliana na maelezo hayo na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa waliobaki maelezo ya mashahidi. Kesi imepangwa Januari 10, 2017.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI