MAMBO MUHIMU YA UCHUNGUZI WA AFYA KWA MWANAUME

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja

Madaktari huunganisha habari unayotoa kutoka kwenye dalili unazohisi, historia ya maradhi yaliyowahi kukusumbua, uchunguzi wa mwili wako pamoja na kufanyiwa vipimo ili kugundua maradhi au hatari ya kupata maradhi fulani kama kisukari.

Kupima afya ni muhimu kwa wanaume, hata kama hawana dalili za magonjwa. Madaktari bingwa wa magonjwa ya tiba wanapendekeza wanaume wafanyiwe uchunguzi wa afya kila mwaka.

Hata hivyo, kama mtu ana viashiria hatarishi vya kupata magonjwa sugu kama kisukari, mtaalamu wa afya atamshauri ni mara ngapi apime afya yake.

Kuna mambo ambayo ni muhimu katika umri wowote na mengine ni muhimu zaidi katika umri mkubwa.

Madaktari huunganisha habari unayotoa kutoka kwenye dalili unazohisi, historia ya maradhi yaliyowahi kukusumbua, uchunguzi wa mwili wako pamoja na kufanyiwa vipimo ili kugundua maradhi au hatari ya kupata maradhi fulani kama kisukari.

Ni vyema kumuuliza daktari wako kuhusu vipimo unavyotakiwa kufanyiwa, kwa maana vipimo hutegemeana na umri, historia ya matatizo ya afya katika familia, mtindo wa maisha unayoishi, vyakula unavyokula, aina ya kazi yako na hali ya unywaji pombe na uvutaji tumbaku.

Unaweza kufanyiwa baadhi ya vipimo kama shinikizo la damu kwenye chumba cha daktari. Vipimo vingine kama Kolonoskopi (Colonoscopy) ambacho ni kipimo kinachotumika kupima saratani ya utumbo mpana, huhitaji vifaa maalumu hivyo inawezekana vikafanyika chumba tofauti.

Vipimo vikubwa zaidi vya afya ya mwili mara nyingi vinahitaji mgonjwa kukaa hospitalini hadi usiku mnene. Vipimo vitafanyika kwenye mwili wako wote ili kuhakikisha huna tatizo lolote. Kama unajisikia vizuri na majibu ya vipimo yameonyesha huna tatizo, basi utakuwa na afya njema.

Kabla ya kufanyiwa vipimo daktari anaweza kushauri usile vyakula vizito kama ugali kwa karibu saa 24, ili kuruhusu baadhi ya vipimo kufanyika. Vipimo vitahusisha X ray za baadhi ya maeneo ya mwili wako kama kifua, vipimo vya mkojo, vipimo vya kinyesi, vipimo vya damu na vinginevyo.

Wakati unafanyiwa vipimo daktari anaweza akawa anakuuliza maswali kadhaa. Na kama una kitu unachohisi ambacho si cha kawaida unaweza kumwambia daktari wako akakufanyia uchunguzi; pengine anaweza kukuandikia dawa nzuri kwa ajili ya maradhi yako. Vipimo gani muhimu kwa wanaume?

SHINIKIZO LA DAMU
Shinikizo la damu linapaswa kupimwa kila unapofika hospitali kwa ajili ya matibabu.

Ikiwa una matatizo ya moyo na figo, na kama una kiharusi, daktari wako atapendekeza uwe na shinikizo la damu la chini zaidi kuliko watu wasio na matatizo.

Inawezekana ukaambiwa kuwa shinikizo lako la damu hupanda kwa vile unazeeka. Hii ni kwa sababu mishipa ya damu inazidi kuwa migumu kwa kadri umri unavyoongezeka.

Shinikizo kubwa la damu siyo zuri kwa afya yako kwa kuwa linaongeza hatari ya kupata kiharusi, mshtuko wa moyo, moyo kushindwa kufanya kazi, ugonjwa wa figo na kifo cha ghafla.

KUPIMA LEHEMU
Kutokana na mfumo wa sasa wa maisha na vyakula tunavyokula, uchunguzi wetu wa kiafya inabidi uhusishe kupima kiwango cha kolesteroli (lehemu).

Kuwa na kiwango kikubwa cha kolesteroli kuna maana ya kuwa na mafuta mengi kwenye damu, kitu kinachoweza kusababisha kupata magonjwa ya moyo.

UZITO NA KIMO
Mtu anapaswa kuwa na uzito unaofaa ambao uko sawa na kimo kwa taratibu za kiafya. Njia sahihi ya kujua kama uzito na kimo chako vipo vizuri kiafya ni kwa kutumia uwiano wa uzito na kimo (BMI).
Unaweza kutumia kikokotozi cha BMI na kupata majibu. Kwa kawaida BMI chini ya 18.5 inaashiria upungufu wa uzito. BMI kati ya 18.5 na 25 huashiria afya njema. Mtu mwenye BMI ya 30 au zaidi atakuwa na uzito kupita kiasi.

UCHUNGUZI WA TEZI DUME
Wanaume wenye miaka kuanzia 45 na kuendelea, wanapaswa kufanyiwa vipimo vya tezi dume. Kipimo rahisi cha kwanza kisicho na gharama ni daktari kuingiza kidole cha shahada katika njia ya haja kubwa na kutomasa tezi dume. Akihisi tezi ni kubwa na ina vinundu, hii ni ishara kuwa una saratani ya tezi dume.

Kipimo kiitwacho kitaalamu Prostate Specific Antigen (PSA) ni kipimo cha damu kinachosaidia kugundua saratani ya tezi dume.

UCHUNGUZI WA UTUMBO MPANA NA PURU
Saratani ya utumbo mpana na puru (njia ya haja kubwa) mara nyingi hutokea wakati kuna uvimbe usio wa kawaida kwenye maeneo hayo.

Vipimo vya kolonoskopi vinaweza kugundua uvimbe mdogo mapema na kuruhusu daktari kuweza kuuondoa kwa upasuaji kabla haujakua.
Kinyesi kilichochanganyikana na damu inaweza kuwa dalili ya mwanzo ya saratani ya utumbo mpana, hivyo kinyesi kinaweza kupimwa kugundua kama kuna saratani hiyo.

Kama umri wako ni chini ya miaka 40, daktari wako anaweza kukufanyia kipimo cha korodani. Daktari atakuambia ugeuze kichwa na ukohoe, huku yeye akishika korodani zako kuangalia henia.

UCHUNGUZI WA MACHO
Ni muhimu kwa wanaume kufanya vipimo vya macho ili kuchunguza matatizo fulani ya macho. Vipimo vinaweza kupima uonaji na afya ya macho yako. Kufanyiwa vipimo vya macho kunaweza kugundua matatizo ya macho kama glaukoma, mtoto wa jicho.

UCHUNGUZI WA MENO
Uchunguzi wa meno unahusisha kukagua meno, fizi, kinywa, ulimi na limfu za shingo. Inashauriwa kufanya uchunguzi wa meno kila baada ya miezi 6 ili kuwa na kinywa chenye afya bora. Ili kukamilisha uchunguzi wa meno, inapaswa kuhusisha vipimo vya X ray.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI