VITUO VYA UTAYARI VYASAIDIA WATOTO WANAOANDIKISHWA DARASA LA KWANZA KUJUIA KUSOMA, KUANDIKA NA KUHESABU SHINYANGA

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja


Kuanzishwa kwa madarasa ya utayari mkoani Shinyanga, kumetajwa kusaidia kuongeza kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza, pamoja na wazazi kupata hamasa ya kuwapeleka watoto wa shuleni.

Hayo yamebainishwa katika kituo cha MWAGALA na kituo cha ILUBALO vilivyopo Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni miongoni mwa vituo vya utayari vilivyoanzishwa chini ya Mpango wa serikali wa kukuza elimu nchini (Equip-Tanzania).


Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Busholi, SEBASTIAN SALAMBA ambayo ni moja ya shule zinazopokea wanafunzi wa darasa la kwanza kutoka katika vituo hivyo, amesema watoto wanaopitia vituo vya utayari wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika.


Mwalimu MARTIN JULIUS wa kituo cha Mwagala na Mwalimu LUCY COSMAS wa kituo cha ILUBALO wameiomba serikali kuwajengea madarasa ya kudumu pamoja na kuwaajiri ili waweze kupata mishahara.


Msimamizi wa vituo hivyo Manispaa ya Shinyanga GIDION STEPHANO amesema sababu kubwa ya kuanzishwa vituo hivyo ni kutokana na umbali wa shule za msingi na kuwepo kwa mito na Mapori yanayotishia usalama kwa watoto.


Kwa upande wake kiongozi wa Equip-Tanzania Mkoa wa SHinyanga, ARCHARD RUYANGE amesema mpaka sasa Equip-Tanzania imepata mafanikio makubwa katika vituo vya utayari ambapo vingine vimepata hadhi ya kusajiliwa na kuwa shule kamili.


Mpango wa Equip-Tanzania ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2019, ulianzishwa na serikali tangu mwaka 2014, na upo katika mikoa Tisa ya Tanzania Bara ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Lindi, Tabora, Kigoma, Mara, Dodoma, Katavi na Singida.

Muonekano wa jengo la kituo cha utayari cha Ilubalo katika kata ya Ibadakuli katika manispaa ya Shinyanga.Kituo hiki kilianzishwa mwaka 2015 kikiwa na watoto 85,mwaka 2016 kilikuwa na watoto 63 na mwaka huu kina watoto 39 ambao wanaandaliwa kuingia darasa la kwanza mwaka ujao

Mwalimu Lucy Cosmas wa kituo cha Ilubalo akicheza na watoto darasani

Mwalimu Lucy Cosmas akiwasimulia hadithi wanafunzi wake

Waandishi wa habari wakiwa ndani ya darasa la mwalimu Lucy Cosmas

Mwalimu akiendelea na somo

Vitabu vya hadithi vinavyotumika kufundishia watoto

Michoro mbalimbali katika kituo cha utayari cha Ilubalo

Mwalimu Lucy Cosmas akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kituo cha utayari cha Ilubalo

Jengo la kituo cha Mwagala katika kijiji cha Bushola kata ya Mwamalili

Mwalimu Martine Julius akiwa na wanafunzi wake katika kituo cha utayari cha Mwagala katika kata ya Mwamalili

Mwalimu Martine Julius akifundisha watoto kuimba

Mwalimu Martine Julius akieleza changamoto zilizopo katika kituo hicho ambazo ni pamoja na paa la jengo kutoboka hali inayosababisha maji kujaa darasani wakati wa mvua lakini pia kituo hicho hakina choo

Wanafunzi wakimsikiliza mwalimu Martine Julius

Waandishi wa habari wakiwa katika darasa hilo

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bushola,Sebastian Pius Salamba akiongea na wanafunzi wa kituo cha utayari cha Mwagala.Shule ya msingi Bushola ndiyo inalea kituo cha utayari cha Mwagala


Mmoja wa wazazi wa watoto wanasoma katika kituo cha utayari cha Mwagala bi Maria Katambi akiwaeleza waandishi wa habari jinsi kituo hicho kinavyosaidia kutoa elimu kwa watoto

Hili ni moja ya madarasa katika shule ya Msingi Ng'wihando iliyopo Old Shinyanga ambayo ni miongoni mwa shule zinazopokea watoto wanaotoka katika vituo mbalimbali vya utayari katika manispaa ya Shinyanga

Wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Ng'wihando wakiwa darasani ambapo waliosimama wametoka katika vituo vya utayari

Mwalimu Mariam Misai akieleza changamoto wanazopata wanafunzi waliotoka katika vituo vya utayari kuwa ni kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni na kuomba serikali kujenga shule katika maeneo ambayo kuna vituo vya utayari

Kiongozi wa Mpango wa kuinua ubora wa elimu nchini (EQUIP – Tanzania) mkoa wa Shinyanga Archard Ruyange akielezea kuhusu faida za kuwa na vituo vya utayari

Kiongozi wa Mpango wa kuinua ubora wa elimu nchini (EQUIP – Tanzania),mkoa wa Shinyanga Archad Ruyange akizungumza na waandishi wa habari

Afisa utamaduni mkoa wa Shinyanga Mariam Ally akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Afisa elimu mkoa wa Shinyanga 


Mkufunzi wa walimu wa madarasa ya utayari wilaya ya Shinyanga Gideon Stephano akizungumza na waandishi wa habari.

Picha zote na Faraji Mfinanga - Dunia Kiganjani Blog

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI