WATUHUMIWA WATATU WAUAWA KWA RISASI NA POLISI

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja

Watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema watu hao waliuawa Jumanne Desemba 5,2017 jioni katika msitu wa Njoro wakati wa majibizano ya risasi na polisi.

Amesema watuhumiwa hao wa ujambazi walikuwa wakiishi chumba kimoja eneo la Njoro ambako polisi walipofika hawakuwakuta na walipata taarifa kuwa wamejificha msituni.

Kamanda Issah amesema kwa kushirikiana na wananchi walikwenda ndani ya msitu huo ambako walisikia milio ya risasi ndipo askari walipofyatua risasi na kusababisha vifo vyao.

Amewataja waliouawa kuwa ni Yusufu Juma Mdoe aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji mwaka 2015; Francis Hamis Kinyaia ‘Wakudata’ ambaye amesema alikuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji mwaka 2013.

Kamanda Issah amemtaja mwingine kuwa ni Valerian Joackim ‘Mdoe’ aliyekuwa na kesi ya mauaji ya mwaka 2013.

Amesema uchunguzi wa polisi umebaini watuhumiwa hao walihusika katika tukio la kufungwa miguu, mikono na kuzibwa mdomo mlinzi lililotokea Novemba 24,2017 eneo la Uru Shimbwe. Katika tukio hilo, bunduki mbili aina ya shotgun ziliporwa.

Kamanda Issah amesema katika msitu wa Njoro walikuta bunduki moja aina ya shotgun iliyokatwa mtutu na kitako, huku namba zikiwa zimefutwa, risasi tatu, maganda matatu ya risasi, mapanga mawili, mkasi unaotumika kukata makufuli, kirungu cha polisi, tindo na misokoto miwili ya bangi.


Ameema miili ya watuhumiwa  imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI