MVUA ILIYONYESHA JUZI YASABABISHA KIFO KATIKA KIJIJI CHA TULOLE WILAYANI KAHAMA

Kama Bado Hujajiunga Nasi, Unaweza Kujiunga Hapa Nikutumie Habari Moja Kwa Moja


MVUA kubwa zilizonyesha juzi usiku zimesababisha kifo cha Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la MARITA MAZIKU (5) aliyeangukiwa na ukuta.

Akizungumza na KAHAMA FM leo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Tulole katika Halmashauri ya Mji wa KAHAMA, SHABAN PASCAL MITUNDU pia amesema nyumba 30 zimebomolewa kufuatia mvua hiyo kubwa.

Sanjari na athari hizo, MITUNDU amesema Nyumba nyingi zimepata nyufa huku zingine zikianguka na kutoa rai kwa wakazi kuhama katika nyumba hizo ili kuepuka maafa zaidi.

Kwa upande wake MAZIKU KULWA ambaye mtoto wake amefariki dunia katika Tukio hilo amesema usiku akiwa amelala na familia yake ghafla alishangaa kuona wamefunikwa ukuta wa nyumba yao huku wakikosa masaada.

Amesema baada ya kupata Msaada kutoka kwa Majirani walipelekwa katika kituo cha Afya cha Igalilimi ambapo walipatiwa matibabu lakini kwa bahati mbaya mwanaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu na mazishi yake yamefanyika jana kijijini hapo.

Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetangaza kuwepo kwa Mvua kubwa katika Mikoa 10 ikiwemo ya kanda ya pwani, kati na nyanda za juu kusini kutokana na ongezeko la mgandamizo wa hali ya hewa kwenye Bahari ya Hindi.

Kupata Habari Na Matukio Ya Kila Siku Bonyeza Like

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI